Pia, mahakama hiyo imetaka mchungaji huyo amlipe fidia ya Sh2 milioni mlalamikaji ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Mbondole iliyoko Ukonga. Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa, Ngomai alianza kumbaka mtoto huyo akiwa na umri wa miaka kumi na moja, wakati huo akisoma darasa la tatu.
Akitoa hukumu hiyo jana, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa Mahakama ya Ilala, Saidi Mkasiwa alisema Mahakama imemtia hatiani mchungaji huyo baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi watano uliotolewa mahakamani hapo akiwamo daktari.
Alisema kutokana na ushahidi huo, upande wa mashtaka ulithibitisha shitaka hilo pasi kuacha shaka, hivyo anamtia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wake. “Mahakama yangu inakutia hatiani kwa kosa la kumbaka mtoto wako, utatumikia kifungo cha maisha jela ili liwe fundisho kwa wazazi wengine wenye tabia mbaya kama yako, pia unatakiwa kumlipa fidia mlalamikaji ya Sh2 milioni,” alisema .
Kabla ya hukumu kutolewa, Wakili wa Serikali, Sylvia Mitanto aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa kwani alitakiwa kuwa mfano bora kwa jamii.
Hata hivyo, mahakama ilitoa nafasi kwa mshtakiwa kujitetea.
Mchungaji huyo aliiomba mahakama itende haki kwani yeye hajui sheria na kosa hilo limetengenezwa halina ukweli wowote.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka iliyosomwa mahakamani hapo, mshitakiwa alitenda kosa hilo kati ya Januari 21, mwaka 2008 katika eneo la Mbondole, Ukonga wilayani Ilala, Dar es Salaam.
Ilidaiwa kuwa mshitakiwa huyo alianza kumbaka mtoto wake huyo akiwa na miaka kumi na moja.
Chanzo: Mwananchi
0 comments