Tuesday, 19 January 2016

Serikali yakiri kosa kutoa leseni ya uchimbaji madini

By    
Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo.
Serikali  imekiri kuwa ilifanya makosa kutoa leseni namba tatu ya uchimbaji wa madini kwa Shanta Mining Tanzania Limited inayochimba dhahabu katika kijiji cha Saza, Chunya mkoani Mbeya.

Kukiri huko kumetokana na baada ya kuwepo kwa mgogoro kati ya wakazi wa kijiji cha Saza na mwekezaji huyo ambaye alipewa leseni ya tatu kwa ajili ya kuendelea na uchimbaji.

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema mwekezaji huyo hakuwa na kosa la kuvamia eneo hilo kwa kuwa alipewa kisheria ila uzembe ulitokea kwa serikali kupitia kwa maofisa wake wanaohusika na utoaji wa leseni.

Prof. Muhongo alisema kutokana na uzembe huo, amemwagiza Kamishna Msaidizi wa Madini nchini, John Nayopa, kwa kushirikiana na maafisa wa madini wa kanda, wilaya na mwekezaji kupitia upya mipaka na kurejesha eneo namba 518 kwa wananchi ili kumaliza mgogoro huo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shanta Mining Limited,  Toby Bradbury, alisema baada ya kukabidhiwa leseni ya tatu, aliomba kufanya mkutano na wananchi lakini walidai kuwa kijijini hapajatulia na kuwa wanaingia kwenye kipindi cha uchaguzi.

Alisema baada ya hapo aliamua kwenda kuwaeleza wananchi wa kijiji cha Mbangala ambao walielimwishwa juu ya upatikanaji wa leseni hiyo na  walielewa bila kuwapo mgogoro kama wa kijiji cha Saza na kwamba tangu waanze shughuli hiyo, hawajawahi kugombana na wanakijiji wa Mbangala.

Alisema kampuni yake inachotaka ni uhusiano mzuri na wananchi, hivyo hata baada ya kurudisha kibali cha utafiti na kupewa cha uchimbaji, walimweleza Ofisa Madini wa Wilaya ya Chunya na walimwomba   afanye mkutano na wanakijiji wa Saza lakini wananchi wakakaidi.

CHANZO: NIPASHE

0 comments