Wakazi 778 wa wilaya za Dodoma na Bahi, hawana makazi baada ya nyumba zao kuanguka kutokana na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana mkoani Dodoma.
Mvua hiyo ilisababisha mafuriko makubwa katika kata za Mpunguzi, Matumbulu, Nzuguni na Dodoma Makulu zote za Manispaa ya Dodoma na Kigwe katika wilaya ya Bahi.
Ofisa Mtendaji wa Kata ya Mpunguzi na Matumbulu, Manispa ya Dodoma, Dionis Samo, alisema zaidi ya nyumba 70 zilianguka na kuacha watu 300 wakiwa hawana makazi pamoja na kuharibu mali, vikiwemo vyakula.
Alisema maji yaliyovunja ukuta wa barabara, yaliingia kwa wingi kwenye makazi ya watu wakiwa wamelala na nyumba nyingi zilianguka kwa sababu zilikuwa za udongo.
“Tatizo hili limekuwa sugu kwani Januari Mosi, mwaka huu, nyumba 48 zilianguka na kufanya watu wengi kukosa makazi. Tatizo la hapa ni mkandarasi wa ujenzi wa barabara ya lami ya Dodoma – Iringa, ambaye alijenga daraja dogo walipohamisha barabara,” alifafanua Samo.
Samo aliongeza kuwa tatizo hilo walishalifikisha serikalini ambapo mkandarasi anatakiwa kurudi kijijini hapo ili kutengeneza miundombinu hiyo upya.
Wakizungumza na waandishi wa habari katika eneo la tukio, wakazi hao walisema mvua hiyo imenyesha usiku na kusababisha uharibifu wa nyumba na mali, hivyo kuwafanya kukosa mahali pa kuishi. Walisema pia hawana chakula kwa kuwa vyakula na mali zingine vilisombwa na maji.
Janeth Mkalabure, mkazi wa Mpunguzi, alisema chanzo kikubwa cha kutokea kwa mafuriko hayo ni midomo ya daraja kuwa midogo hali inayosababisha maji kuacha kufuata mkondo na kuingia katika makazi ya watu.
Agness Kabogo, alisema katika mtaa wao wa Sabasaba katika kata ya Mpunguzi, zaidi ya nyumba 15 zimeanguka na kusababisha baadhi ya wananchi kukosa mahali pa kuishi.
Naye Diwani wa Kata ya Kigwe, Paschal Sijila, alisema nyumba 270 zilianguka katika kata yake na watu 460 hawana mahali pakuishi.
Sijila alisema mafuriko hayo ni ya mara ya pili katika kipindi cha mwaka huu ambapo ya awamu hii yalikuwa zaidi licha ya kuwa walikuwa bado wanafanya tathmini ya uhalibifu wa mali uliojitokeza awali.
Katika kata ya Dodoma Makulu kulikuwa na tatizo kama hilo na Diwani wa Kata hiyo, Paschal Matula, alisema nyumba 18 zimeanguka kutokana na maji yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha usiku wa kuamkia jana, hivyo msaada wa haraka unahitajika.
CHANZO: NIPASHE
0 comments